Mabinti Pacha Walioungana Kuhitimu Kidato cha Nne
Hatua ya kwanza ya ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha
walioungana kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha
Ikonda wilayani Makete mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa kutimia Novemba
mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu kidato
cha nne.
Itakumbukwa kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009
kijijini kwao Ikonda, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao
kwa pamoja walisema wanataka kuwa wasomi waliobobea katika utaalamu wa
kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu
Muhtasi.
Wanafunzi hao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es Salaam.
Kwa sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari
Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika
mazingira magumu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni,
walisema wanafurahi kuwa miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani
huo wa kidato cha nne mwaka huu.
“Tunafurahi, tunajiandaa tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu
tunataka tufaulu vizuri masomo yetu, ili ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu
Muhtasi itimie,” walisema Maria na Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia wana kiti maalumu.
Pacha hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila
mmoja ana madaftari yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi
wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
“Wala hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake,
mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa
kulia,” anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Ilianzishwa mwaka 2006 na hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote
wanaishi kituoni hapo na wote wanatoka kwenye mazingira magumu.
Changamoto kubwa iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya
umeme, ambapo uongozi wa shule na kituo hicho unalazimika kutumia
jenereta na umemejua, jambo ambalo mapema wiki hii Wakala wa Nishati ya
Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa kuwapelekea umeme.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Iringa.
Walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja
alipata alama 151, ingawa walitofautiana ufaulu kwenye masomo yao.
Katika somo la Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na
Maria alama 25, kwenye somo la Kiingereza, Maria alipata alama 36 na
kumzidi Consolata aliyepata alama 34, wakati kwenye somo la Sayansi,
Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga
na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es
Salaam.
Hata hivyo hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na
pia umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao
wakawachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996.
Lakini, taarifa zao hazikufahamika hadi pale walipoandikishwa kuanza
elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya
wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado wadogo.
0 comments: